Amisom: Tumekomboa 80% ya maeneo yaliyokuwa chini ya al-Shabaab Somalia
Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia Amisom kimesema kimefanikiwa kukomboa asilimia 80 ya maeneo ambayo yalikuwa kwenye makucha ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Hayo yaliarifiwa jana Alkhamisi katika mkutano wa wakuu wa majeshi na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizochangia askari wa Amisom, walipokutana mjini Kampala, Uganda kujadili kuhusu mikakati ya kuimarisha amani na usalama nchini Somalia.
Akihutubia mkutano huo jana, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uganda, Sam Kutesa amesema ameitaka jamii ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Amisom, ili mafanikio yaliyopatikana na kikosi hicho hasiambulie patupu.
Hii leo Rais Yoweri Museveni wa Uganda atakuwa mwenyeji wa marais wenzake kutoka nchi za Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopia, nchi zinaounda kikosi cha Amisom chenye askari zaidi ya 21 elfu.
Kundi la al-Shabaab lilikuwa likidhibiti maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia lakini lilipokonywa maeneo hayo muhimu, ikiwemo miji mikubwa ambayo ilikuwa mikononi mwa wanachama wa genge hilo mwaka 2015 kufutia operesheni nzito zilizofanywa na jeshi la Somalia kwa kushirikiana na askari wa Amisom.
Kikosi cha Amisom ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007.