Sudan Kusini yaomba uanachama Arab League
Sudan Kusini jana Jumanne iliwasilisha ombi rasmi la kuwa mwanachama katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).
Ombi hilo la Sudan Kusini limepangwa kujadiliwa leo katika kikao cha 149 cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya hiyo huko Cairo nchini Misri. Baada ya kujitenga Sudan Kusini na nchi ya Sudan, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitangaza kuwa nchi hiyo inaweza kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo, lakini kwamba inapasa kutangaza lugha ya Kiarabu kama lugha yake rasmi. Lugha rasmi inayotumika nchini humo ni Kiingereza.
Sudan Kusini ina uhusiano mzuri na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Misri na viongozi wa Khartoum wanautambua utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ndiyo chanzo cha kujitenga Sudan Kusini na Sudan.
Sudan Kusini ilipata uhuru ilipojitenga na Sudan tarehe 9 mwezi Julai mwaka 2011. Licha ya kuwa na maliasili ya mafuta, Sudan Kusini ni moja ya nchi maskini zaidi duniani. Nchi hiyo ina jamii ya watu karibu milioni 12 na asilimia 90 wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Nchi hiyo inaendelea kushuhudia mapigano kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na wale wa kiongozi wa waasi Riek Machar.