Watu 16 wauawa kwa kupigwa na radi kanisani nchini Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41507-watu_16_wauawa_kwa_kupigwa_na_radi_kanisani_nchini_rwanda
Kwa akali watu 16 wamepoteza maisha baada ya kupigwa na radi wakiwa kanisani huko kusini mwa Rwanda, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Burundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2018 12:55 UTC
  • Watu 16 wauawa kwa kupigwa na radi kanisani nchini Rwanda

Kwa akali watu 16 wamepoteza maisha baada ya kupigwa na radi wakiwa kanisani huko kusini mwa Rwanda, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Burundi.

Habitegeko Francois, Meya wa mji wa Gihemvu, wilaya ya Nyaruguru katika Mkoa wa Kusini ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, tukio hilo lilitokea jana, ambapo Wakristo wa madhehebu ya Sabato (SDA) walikuwa wamekusanyika kanisani kama ada yao ya kukusanyika kwa ajili ya ibada zao siku za Jumamosi.

Amesema watu 14 waliaga dunia papo hapo baada ya radi hiyo kupiga kanisa la SDA, huku wengine wawili wakipoteza maisha kwa majeraha walipokuwa wakitibiwa hospitalini.

Kanisa nchini Rwanda

Amesema watu wengine 140 wamejeruhiwa katika tukio hilo na kupekekwa hospitalini, baadhi yao wakiruhusiwa kwenda nyumbani hii leo. Duru za hospitali zinasema watatu miongoni mwa majeruhi ndio wapo katika hali mahututi.

Kwa mujibu wa meya huyo, tukio jingine kama hilo lilitokea siku ya Ijumaa kusini mwa Rwanda, ambapo wanafunzi 18 walijeruhiwa na mmoja kufariki dunia kwa kupigwa na radi.