Kuanza uchaguzi wa rais nchini Misri, viashiria hasi vya uchaguzi
Uchaguzi wa rais wa Misri ulianza jana Ijumaa machi 16 kwa Wamisri wanaoishi katika nchi 124 za kigeni na utaendelea kwa muda wa siku tatu.
Uchaguzi huo utaanza kufanyika ndani ya Misri katika kipindi cha siku 9 zijazo yaani tarehe 26 ya mwezi huu wa Machi na kuendelea kwa siku tatu. Rais Abdulfattah as-Sisi na Musa Mustafa wa chama cha al-Ghad wanachuana katika uchaguzi huo. Kuna mambo yanayofanyika katika uchaguzi huo ambayo yamepunguza itabari yake. Jambo muhimu la kwanza ni kwamba hatua zimechukuliwa kuhakikisha kwamba hakuna ushindani wala upinzani mkali unaotolewa dhidi ya rais wa hivi sasa wa Misri yaani, Abdufattah as-Sisi na kwa hivyo kiongozi huyo tayari amedhaminiwa ushindi na fursa ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mingine minne. Tayari wabunge 540 kati ya wabunge wote 593 wa Misri wametangaza kumuunga mkono Rais as-Sisi.
Hivyo wakosoaji wanamini kwamba hakuna mazingira yoyote ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki nchini humo kwa sasa kwa sababu wapinzani wakuu wote wa as-Sisi wamekwishafutwa na serikali katika medani ya uchaguzi kwa kuzushiwa tuhuma zisizo na msingi. Hata baadhi ya wajuzi wa mambo wanasema kuwa Musa Mustafa amesukumwa kwenye uchaguzi huo ikiwa ni katika juhudi za kuwafumba macho na kuwafanya waone kuwa uchaguzi huo umekuwa na ushindani unaokubalika. Kwa msingi huo kuna uwezekano wa uchaguzi huo kususiwa na baadhi ya makundi, wanasiasa na matabaka tofauti ya wananchi. Hata hivyo Abdul Amir Nabawi, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati anasema kuwa ususiaji huo hauwezi kuwa na athari yoyote katika mkondo wa kufanyika na kutangazwa matokeo ya uchaguzi.
Kiashiria kingine hasi cha uchaguzi wa mwaka huu wa Misri ni kuwa licha ya kuwepo ufa na mgawanyiko katika jehi la taifa, lakini jambo lisilo na shaka ni kuwa wanajeshi bado wana nafasi muhimu na ya msingi katika kuainisha mkondo wa uchaguzi. Kabla ya kuwa rais wa Misri mwaka 2014, Jenerali as-Sisi alikuwa tayari amehudumia vyeo mbalimbali vya ngazi za juu jeshini na hata ndiye aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013 dhidi ya Muhammad al-Mursi, rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia. Hata kama wanajeshi waliowengi wanamuunga mkono as-Sisi katika uchaguzi huu lakini hatua ya Sami Annan, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Misri, ya kujiandikisha kugombea nafasi ya rais katika uchaguzi huo, inabainisha wazi kupungua kiwango cha kuwepo msimamo mmoja jeshini kwa maslahi ya as-Sisi. Kiashiria cha tatu hasi kuhusu uchaguzi wa rais wa Misri mwaka huu ni kuwa kwa kutilia maanani mbinu ya kuwafuta wagombea wapinzani, uchaguzi huu hawezi kuchukuliwa kuwa ni kipimo cha kupima utendaji wa serikali ya as-Sisi katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Kuhusu hilo Abdul Ami Nabawi anasema kwamba kwa kuzingatia kuwa msindi wa uchaguzi huo, yaan Rais as- Sisi, tayari amejulikana hata kabla ya kufanyika uchaguzi wenyewe, uchaguzi huu unafanana moja kwa moja na uchaguzi mwingine wa kimaonyesho uliandaliwa nchini humo mwaka 2005, ambapo rais wa wakati huo Husni Mubarak alidai kuandaa uchaguzi wa kwanza kidemokrasia katika hali ambayo ilijulikana wazi hata kabla ya kufanyika uchaguzi, kuwa ndiye aliyekuwa mshindi. Ukweli wa mambo ni kuwa wananchi wa Misri wanaelekea katika vituo vya kupigia kura katika hali ambayo hawatarajii kutokea mabadiliko yoyote ya utendaji serikalini katika miaka minne ijayo, bali hata mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo yanatazamiwa kuendelea kumdhaminia as-Sisi uongozi katika chaguzi nyingine zijazo.