Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya yatoa onyo kwa wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4198-serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_ya_libya_yatoa_onyo_kwa_wapinzani
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeonya kuwa itakabidhi majina ya wapinzani wa serikali hiyo kwa Polisi ya Kimataifa Interpol na kuwahusisha na "ugaidi" endapo hawatotoa ushirikiano kwa serikali hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2016 23:55 UTC
  • Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya yatoa onyo kwa wapinzani

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeonya kuwa itakabidhi majina ya wapinzani wa serikali hiyo kwa Polisi ya Kimataifa Interpol na kuwahusisha na "ugaidi" endapo hawatotoa ushirikiano kwa serikali hiyo.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imesisitiza kuwa itatuma majina hayo ya watu 17 wakiwemo wanasiasa, viongozi wa wanamgambo na shakhsia wa kidini kwa Polisi ya Kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwahusisha na "kuunga mkono ugaidi" endapo wataendelea "kukwamisha mchakato wa demokrasia".

Miongoni mwa waliotajwa katika orodha hiyo ni Khalifa al-Ghawi, Waziri Mkuu wa serikali yenye makao yake katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, Spika wa Bunge Nouri Abu Sahmain na Mufti al-Sadeq al-Ghariani, aliyejitangaza mkuu wa kidini wa serikali hiyo.

Onyo hilo limetolewa siku moja baada ya Waziri Mkuu mteule Fayez al-Sarraj pamoja na maafisa wengine sita wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kuwasili nchini humo kwa boti wakitokea Tunisia katika jitihada za kufanikisha ushikaji hatamu za madaraka wa serikali hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni, serikali iliyojitangaza mjini Tripoli ambayo haitambuliwi na Jamii ya Kimataifa, pamoja na makundi yanayobeba silaha yanayoiunga mkono zilitoa onyo la kuitaka serikali ya Umoja wa Kitaifa isitie mguu wake katika mji mkuu huo wa Libya.../