Apr 01, 2016 07:14 UTC
  • Ban apongeza kuingia Tripoli Baraza la Urais la Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha kuwasili kwa Baraza la Urais la Libya mjini Tripoli mnamo Machi 30, 2016, akitaja kuwasili huko kama hatua muhimu katika kutekeleza makubaliano ya kisiasa ya Libya.

Akizungumza Alhamisi, Ban ametoa wito kwa wadau kuheshimu matamanio ya raia wengi wa Libya ya amani, ustawi na mafanikio.

Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa wadau wote na taasisi za umma zisaidie kuwezesha kukabidhi madaraka kwa njia ya amani, akikumbusha wajibu wa wale wanaosimamia usalama kuhakikisha usalama wa Baraza la Urais, na kuwahimiza wajiepushe na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga kazi ya baraza hilo.

Ban amepongeza Baraza la Urais kwa ujasiri na uongozi wake, na kukariri kuwa tayari Umoja wa Mataifa kusaidia mamlaka na watu wa Libya, ili nchi yao iendelee kupiga hatua kwenye barabara ya mpito wa kidemokrasia.

Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio la kuongeza muda wa mamlaka ya vikwazo ilivyowekewa Libya chini ya azimio lake namba 2146 la mwaka 2014, hadi Julai 31 mwaka 2017. Baraza la Usalama pia limelaani majaribio ya uuzaji haramu wa mafuta ghafi ya Libya nje, ukiwemo ule unaofanywa na taasisi ambazo hazipo chini ya mamlaka ya serikali ya makubaliano ya kitaifa (GNA). Azimio hilo pia limeitaka serikali ya Libya kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu bandari, visima vya mafuta na majengo yaliyo chini ya mamlaka yake, na kuhusu njia zinazotumiwa kuhakiki uuzaji halali wa mafuta ghafi nje, pamoja na uagizaji na uuzaji wa silaha.

Tags