Ripoti: Vijana wamesusia uchaguzi wa rais Misri
Ripoti zinaonesha kuwa, idadi kubwa ya vijana wa Misri hawakupiga kura katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Ripoti zinaonesha kuwa, idadi kubwa ya vijana wa Misri ambao wanaunda asilimia 60 ya jamii ya nchi hiyo na karibu nusu ya watu waliokamilisha masharti ya kupiga kura wamepuuza uchaguzi wa rais uliofanyika Jumatatu iliyopita na kwamba wapigaji kura wengi walikuwa wazee na watu wazima.
Vijana wengi wa Misri wamesusia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo licha ya Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo kufanya kampeni kubwa za kuwashawishi vijana wampigie kura.
Mbali na kizazi cha vijana, uchaguzi wa rais wa Misri pia ulisusiwa na vyama vyote vikuu vya upinzani baada ya wagombea wengi wa vyama hivyo ama kuzuiwa kugombea au kuswekwa jela kabla kidogo ya uchaguzi huo.
Uchaguzi huo uliwashirikisha wagombea wawili tu yaani jenerali mstaafu Abdel Fattah al Sisi na Moussa Mostafa Moussa ambaye pia anaaminika kuwa ni muungaji mkono na al Sisi.
Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ametangazwa mshindi wa uchaguzi huo tata wa rais kwa kuzoa asilimia 92 ya kura zote zilizopigwa.