EU yawawekea vikwazo viongozi wanaopinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4261-eu_yawawekea_vikwazo_viongozi_wanaopinga_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_libya
Umoja wa Ulaya EU umeanza kutekeleza mpango wa kuwawekea vikwazo viongozi wa kisiasa wanaopinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2016 01:46 UTC
  • EU yawawekea vikwazo viongozi wanaopinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya

Umoja wa Ulaya EU umeanza kutekeleza mpango wa kuwawekea vikwazo viongozi wa kisiasa wanaopinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya.

Viongozi wa Libya wanaokabiliwa na vikwazo hivyo vya kiuchumi na ambao tayari akaunti zao za benki zimefungwa ni Nouri Abusahmain, mkuu wa chama cha Kongresi cha serikali ya Tripoli, Khalifa al-Ghwell, Waziri Mkuu wa serikali ya Tripoli na Aguila Saleh ambaye ni rais wa bunge la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika linalotambulika kimataifa.

Taarifa ya EU imesema kuwa, viongozi wa umoja huo wamewachukulia hatua hiyo kali wanasiasa hao wa Libya kwa kuwa kizingiti kikubwa katika mchakato wa kuafikiwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Machi 30, Baraza la Urais la Libya liliwasili mjini Tripoli kwa meli, hatua ambayo ilipongezwa na Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki-Moon alitoa wito kwa wadau kuheshimu matakwa ya raia wengi wa Libya ya amani, ustawi na mafanikio.

Hii ni katika hali ambayo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeonya kuwa itakabidhi majina ya wapinzani wa serikali hiyo kwa Polisi ya Kimataifa Interpol na kuwahusisha na "ugaidi" endapo hawatotoa ushirikiano kwa serikali hiyo. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imesisitiza kuwa itatuma majina ya watu 17 wakiwemo wanasiasa, viongozi wa wanamgambo na shakhsia wa kidini kwa Polisi ya Kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuwahusisha na "kuunga mkono ugaidi" endapo wataendelea "kukwamisha mchakato wa demokrasia".