Ajali mbaya ya gari, watu 12 wafariki dunia Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42680
Kwa akali watu 12 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya basi iliyotokea  mkoani Tabora nchini Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti, ajali hiyo imelihusisha basi la Kampuni ya City Boys lililogongana na lori aina ya Fuso katika eneo la Makomero wilaya ya Igunga mkoani Tabora na kwamba ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 05, 2018 08:15 UTC
  • Ajali mbaya ya gari, watu 12 wafariki dunia Tanzania

Kwa akali watu 12 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya basi iliyotokea  mkoani Tabora nchini Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti, ajali hiyo imelihusisha basi la Kampuni ya City Boys lililogongana na lori aina ya Fuso katika eneo la Makomero wilaya ya Igunga mkoani Tabora na kwamba ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo.

Aidha mbali na watu 12 kufariki dunia, wengine 46 wamejeruhiwa, baadhi wakiwa mahututi. Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Tabora, Inspekta Hardson, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni tairi la kulia la gari ya Fuso kupasuka wakati dereva akijaribu kukwepa shimo na kupoteza mwelekeo na hivyo kugongana na basi la City Boys uso kwa uso.

Moja ya ajali mbaya zilizowahi kutokea nchini Tanzania

Hardson amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Igunga huku baadhi ya majeruhi wakiwa wamepelekwa katika hospitali ya Nkinga na Bugando mkoani Mwanza kwa ajili ya matibabu. Ongezeko la ajali za barabarani nchini tanzania linatajwa kusababishwa na madereva kutoheshimu sheria za barabarani ambapo hivi karibuni pia, yaani tarehe 24 mwezi uliopita kulitokea ajali mbaya mkoani Pwani na kusababisha watu 26 kupoteza maisha. Takwimu zinaonyesha kuwa, kila mwaka mamia ya watu hufariki dunia katika ajali za namna hiyo nchini Tanzania suala lililoifanya polisi ya nchi hiyo kuweka sheria kali za barabarani kukiwemo kuwatoza faini kubwa madereva.