Misri, Sudan na Ethiopia zashindwa kuafikiana kuhusu bwawa la al-Nahdha
(last modified Fri, 06 Apr 2018 14:20:18 GMT )
Apr 06, 2018 14:20 UTC
  • Misri, Sudan na Ethiopia zashindwa kuafikiana kuhusu bwawa la al-Nahdha

Mkutano wa Misri, Sudan na Ethiopia wa kujadili suala tata la bwawa la al-Nahdha umegonga mwamba huku pande tatu hizo zikishindwa kuafikiana.

Ibrahim Ghandour, Waziri wa Mambo ya Nje ya Sudan amesema leo Ijumaa kuwa, mazungumzo ya masaa 15 yaliyofanyika mjini Khartoum kuhusu bwala wa al-Nahdha katika Mto Nile yamemalizika bila kufikia natija yoyote.

Amesema mkutano huo mbali na kuwaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tatu hizo, lakini pia umehudhuriwa na mawaziri wa kilimo na wakuu wa idara za kiintelijensia.

Bwala la al-Nahdha

Februari mwaka huu, Misri ilikubali ombi la Ethiopia la kutaka kuakhirisha mkutano wa pande mbili wa kujadili suala tata la bwawa la al-Nahdha linalojengwa na Uhabeshi, baada ya Adiss Ababa kutangaza sheria ya hali ya hatari.

Misri imekuwa ikipinga mradi wa Ethiopia wa kujenga bwawa la al-Nahdha ambalo litatumia maji ya Mto Nile katika miradi yake ya maendeleo, ikihofia kuwa utapunguza maji ya mto huo na kusababisha ukame na upungufu wa maji ya kunywa nchini humo. Mgogoro huo ulishtadi baada ya Misri kuituhumu Sudan kuwa inaiunga mkono Ethiopia katika mradi wake huo.

 

Tags