Rais Pierre Nkurunziza alifanyia marekebisho baraza lake la mawaziri Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43392-rais_pierre_nkurunziza_alifanyia_marekebisho_baraza_lake_la_mawaziri_burundi
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2018 09:47 UTC
  • Rais Pierre Nkurunziza alifanyia marekebisho baraza lake la mawaziri Burundi

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais imesema kwamba, katika mabadiliko hayo Rais Nkurunziza amewafuta kazi mawaziri wanne. Kadhalika Rais huyo amewateua mawaziri wapya watano na kuongeza idadi ya mawaziri wa serikali yake kutoka 20  hadi 21. Kwa mujibu wa habari hiyo, mabadiliko hayo yalifanywa jana Alkhamisi. Kubadilishwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, ni kati ya mabadiliko yaliyofanywa na Rais Pierre Nkurunziza. Hii ni kusema kuwa kuwa, nafasi ya Alain-Aimé Nyamitwe, Waziri wa Mambo ya Nje, imechukuliwa na Ezechiel Nibigira, tawi la vijana la chama tawala CNDD-FDD.

Aimé Nyamitwe, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Burundi

Nyamitwe alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi tangu mwezi Mei 2015, yaani mara baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Mabadiliko hayo yamejiri ikiwa umesalia mwezi mmoja kabla ya kufanyika kura ya maoni ambayo itatoa fursa kwa Rais Nkurunziza kubakia madarakani kwa muda mrefu zaidi yaani hadi mwaka 2034. Burundi imekumbwa na mgogoro wa ndani tangu April 2015, baada ya rais huyo kutangaza kugombea katika uchaguzi wa rais uliopita ambao aliibuka mshindi nchini humo.