Kubadilishwa jina la Swaziland, sasa yaitwa eSwatini
Mfalme wa Swaziland amebadili jina la nchi hiyo na kuwa eSwatini kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 50 wa kukomeshwa ukoloni wa Uingereza nchini humo.
Mfalme Mswati III wa Swaziland amesema katika sherehe za kuadhimisha mwaka wa 50 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kwamba, tofauti na nchi nyingi za Afrika, Swaziland haukubadilisha jina lake baada ya kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza na swala hilo linafanyika mwaka huu. Awali nchi tatu za kusini mwa Afrika zilizojulikana kwa majina ya Rhodesia, Nyasaland na Bechuanaland zilibadili majina yao na kuwa Zimbabwe, Malawi na Botswana baada ya kupata uhuru.
Jina la Swaziland ambalo linaundwa na sehemu mbili za kienyeji na Kiingereza, limekuwa likiwakasirisha sana raia wa nchi hiyo. Kubadilishwa kwa jina hilo kunafanyika katika zama hizi ambapo wakazi wengi wa Afrika wamekuwa wakipinga uingiliaji kati na ushawishi wa nchi za kikoloni za Magharibi katika masuala ya bara hilo. Si hayo tu bali hata viongozi wa nchi za Magharibi wenyewe wanakiri kwamba, nchi hizo zimetenda jinai na uhalifu barani Afrika. Kwa mfano tu hivi karibuni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema kuwa: "Wakoloni wa Ulaya walifanya jinai barani Afrika na suala hilo ni uhakika usio na shaka ndani yake. Kumefanyika jinai na makosa barani Afrika."
Afrika siku zote imekuwa ikitazamwa na madola makubwa kama chanzo cha malighafi zenye thamani kubwa. Afrika daima inakodolewa macho na Wamagharibi kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya almasi, dhahabu, mafuta na kadhalika na ina nafasi muhimu katika jiografia ya kisiasa inayotumiwa kwa ajili ya kutimiza stratijia za nchi za wakoloni. Kwa msingi huo nchi za Magharibi zimekuwa zikipora utajiri na maliasili ya Afrika na kulazimisha siasa za kikoloni kwa serikali na tawala za Kiafrika, siasa ambazo zinapalili ujinga, umaskini na tawala fisadi na za kidikteta ambazo zinahudumia maslahi na malengo yao. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Waafrika wengi wanachukia siasa za nchi hizo za kikoloni ambazo hadi hii leo zinatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha zinaendelea kudhibiti siasa, utajiri na maliasili za Afrika. Mchambuzi wa siasa za Afrika, Pierre Dogbou anasema: Kuna udharura kwa nchi za Afrika kujiondoa katika mzingo wa siasa za kijuba za kipindi cha ukoloni na kuanzisha mazingira mapya yatakayoliingiza bara hilo katika kipindi na awamu mpya.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, katika miongo mitatu iliyopita moyo wa mapambano dhidi ya siasa za kikoloni na dhulma za madola makubwa ya kibeberu umeshika kasi zaidi katika nchi za Kiafrika kutokana na kuongezeka mwamko wa kisiasa na mabadiliko ya hali ya kiuchumi na kiutamaduni katika nchi nyingi za bara hilo. Kwa sasa Walimwengu wengi hawakubali kabisa ukoloni mamboleo na wanafanya jitihada kubwa za kung'oa kabisa athari mbaya ziliaobakishwa nyuma na ukoloni wa zamani. Hatua ya Swaziland ya kubadili jina la kipindi cha ukoloni la nchi hiyo ni mfano hai wa ukweli huo.