EAC na Interpol zaandaa warsha ya kupambana na magendo ya binadamu, mihadarati
(last modified Tue, 24 Apr 2018 16:35:17 GMT )
Apr 24, 2018 16:35 UTC
  • EAC na Interpol zaandaa warsha ya kupambana na magendo ya binadamu, mihadarati

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Polisi ya Kimataifa (Interpol) zimeandaa warsha ya siku saba visiwani Zanzibar nchini Tanzania, inayojadili mbinu za kupambana na magendo ya binadamu na dawa za kulevya katika eneo hilo.

Taarifa ya sektritariati ya EAC imesema lengo la jumuiya hiyo na Interpol kuandaa warsha hiyo ya pamoja iliyoanza jana Jumatatu ni kujadiliana na kubadilishana mawazo juu ya njia za kupanua elimu ya kukabiliana na magendo ya binadamu na mihadarati katika kanda ya Afrika Mashariki.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanatumai kwamba mwishoni mwa mkutano huo unaotazamiwa kumalizika Aprili 28, wataweza kuja na ramani ya njia ya kupambana na magendo hayo na kutathmini mambo ambayo yamekuwa kizingiti katika kutekelezwa Sheria ya Kukabiliana na Mihadarati/Binadamu ya jumuiya hiyo.

Bandera za nchi wanachama wa EAC

Charles Njoroge, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa la jumuiya hiyo amesema wanawake wamekuwa wahanga wakuu wa magendo ya mihadarati na utumwa mamboleo katika kanda ya Afrika Mashariki.

Amesema mbali na magendo ya binadamu na mihadarati, nchi za kanda ya Afrika Mashariki zinakabiliwa na biashara haramu ya kuingizwa katika nchi hizo chakula na dawa ambazo ni ghushi na muda wake wa matumizi umepita.  

Tags