Mvua na maporomoko ya ardhi yaendelea kusababisha maafa nchini Rwanda
Serikali ya Rwanda imesema watu wengine 18 wamefariki dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo.
Wizara inayohusika na kupambana na majanga ya kimaumbile nchini humo imesema kuwa, watu hao waliaga dunia usiku wa kuamkia jana katika maeneo tofauti ya nchi.
Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa wizara hiyo imesema kuwa, watu saba miongoni mwao walipoteza maisha kaskazini mwa nchi, wanane katika mji mkuu Kigali na watatu katika eneo la Gatsibo, mashariki mwa nchi.
Kadhalika nyumba 79 zimesombwa na mafuriko hayo, huku mimea katika mashamba ya hektari 56 ikiharibiwa kikamilifu.
Wizara inayohusika na kupambana na majanga ya kimaumbile nchini humo imesema kuwa, inaendelea kuwahamasisha watu wanaoishi kwenye maeneo ya mabonde kuhamia nyanda za juu.
Mwezi uliopita watu 16 walifariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi walipokuwa kanisani jimbo la magharibi nchini humo.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali, kati ya Januari mwaka huu na katikati ya mwezi Aprili, watu 51 waliaga dunia kutokana na athari za majanga hayo ya kimaumbile nchini Rwanda.