Al Sisi aahidi kuhitimisha oparesheni za jeshi huko Sinai
(last modified Sun, 29 Apr 2018 07:40:28 GMT )
Apr 29, 2018 07:40 UTC
  • Al Sisi aahidi kuhitimisha oparesheni za jeshi huko Sinai

Rais wa Misri ametangaza kuwa oparesheni za jeshi la nchi hiyo katika mkoa wa Sinai ya Kaskazini zitahitimishwa hivi karibuni.

Al Abdel Fattah al Sisi jana aliahidi kwamba oparesheni za kijeshi dhidi ya makundi yanayobeba silaha katika Peninsula ya Sinai zitahitimishwa siku chache zijazo. Rais huyo hata hivyo hakusema ni lini oparesheni hizo zitasitishwa. Jeshi la Misri katika miezi ya karibuni lilianzisha oparesheni kubwa kwa ajili ya kukabiliana na makundi yenye silaha ya wanamgambo na magaidi likiwemo kundi la Daesh katika mkoa wa Sinai ya Kaskazini. 

Magaidi wa kundi la Daesh katika Peninsula ya Sinai nchini Misri 

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa, karibu wanachama 200 wa kundi hilo na wanajeshi wa Misri wasiopungua 33 wameuawa tangu kuanza kwa oparesheni hizo za kijeshi dhidi ya tawi la kundi la Daesh linaloendesha hujuma huko Misri. 

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, wanajeshi 8 wa Misri na magaidi 14  waliuawa katikati mwa mwezi huu wa Aprili katika mapigano yaliyotokea katikati mwa Peninsula ya Sinai wakati watu wenye silaha waliokuwa wamejizatiti kwa maguruneti walipokivizia kivuko cha jeshi katika eneo hilo.

Shambulio hilo lilitajwa kuwa kubwa zaidi dhidi ya askari usalama wa Misri tangu Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo ashinde kiti cha urais kwa muhula wa pili mwezi uliopita.

Tags