Mahakama yamuuzulu Waziri Mkuu na kuvunja Bunge Gabon
Mahakama ya Katiba nchini Gabon imeagiza kuvunjwa kwa Bunge la Taifa la nchi hiyo sanjari na kumuuzulu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, hatua ambayo imesitisha shughuli za serikali ya Rais Ali Bongo wa nchi hiyo.
Rais wa mahakama hiyo, Marie Magdeleine Mborantsuo amesema jukumu la wabunge hao limefikia ukiongoni kwa kuwa serikali imeshindwa kufanya uchaguzi wa Bunge.
Februari mwaka huu, Alain-Claude Bilie By Nze, msemaji wa serikali ya Gabon ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano alitangaza kuwa uchaguzi wa Bunge ungefanyika tarehe 28 ya mwezi uliopita wa Aprili.
Awali uchaguzi wa Bunge nchini Gabon ulipangwa kufanyika Disemba mwaka 2016, lakini ukaakhirishwa kutokana na mazingira yaliyokuwa yakitawala nchini humo ambayo hayakuruhusu kufanyika uchaguzi huo.
Mahakama ya Katiba ya Gabon kadhalika ameliagiza Bunge la Seneti la nchi hiyo kusimamia shughuli za Bunge la Taifa, hadi uchaguzi utakapofanyika.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo Emmanuel Issoze-Ngondet amekubali agizo la mahakama hiyo la kumtaka ajiuzulu huku akisisitiza kuwa, 'maamuzi ya mahakama sio jambo lenye mjadala bali yanapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa.'
Issoze-Ngondet aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Rais Bongo baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, ambao waangalizi wa kimataifa walisema kuwa uligubikwa na kasoro nyingi na kuzusha machafuko.