Serikali ya Misri yalaumiwa kwa kuwatesa wafungwa
(last modified Mon, 07 May 2018 15:06:10 GMT )
May 07, 2018 15:06 UTC
  • Serikali ya Misri yalaumiwa kwa kuwatesa wafungwa

Shirika la Kimataifa la Msahama Duniani la Amnesty International limelaani mateso wanayofanyiwa wafungwa na serikali ya Misri ikiwa ni pamoja na kuwekwa wafungwa wa kisiasa kwenye seli za mtu mmoja mmoja kwa muda mrefu na kusema kuwa, huo ni ushahidi wa wazi wa namna serikali ya Rais Abdul Fattah el Sisi inavyowatesa wafungwa nchini humo.

Katika ripoti yake mpya kabisa iliyotolewa leo Jumatatu, shirika la Amnesty International limesema, makumi ya wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wapinzani wa serikali ya Misri wametiwa mbaroni na kufanyiwa vitendo vya kinyama mno katika seli za mtu mmoja mmoja wakiwa jela.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, hatua hiyo ya serikali ya Misri imewasababishia wafungwa hao matatizo ya kisaikolojia, kuwa na hofu muda wote na kuwa na matatizo katika kumbukumbu zao na kushindwa kuzingatia mambo kwa umakini wa kutosha.

Rais wa Misri, Jenerali Abdul Fattah el Sisi

 

Shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza limeongeza kuwa, tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013 yaliyomuondoa madarakani Mohammad Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuwahi kuchaguliwa kidemokrasia hadi hivi sasa, mamia ya maelfu ya watu wameshatiwa mbaroni na kuwekwa korokoroni huko Misri.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata Mohammad Morsi mwenyewe amekuwa akishikiliwa kwenye seli ya mtu mmoja mmoja katika jela moja ya Misri kwa miaka mitano sasa.

Rais wa hivi sasa wa Misri, Abdul Fattah el Sisi aliteuliwa na Mohammad Morsi kuwa mkuu wa jeshi la nchi hiyo, lakini alimgeuka na kuongoza mapinduzi ya kijeshi mwaka 2013 na baadaye kumshikilia korokoroni Morsi hadi leo hii.

Tags