Operesheni ya kuukomboa mji wa Derna yaanza nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44186-operesheni_ya_kuukomboa_mji_wa_derna_yaanza_nchini_libya
Kamanda wa timu ya operesheni ya jeshi la Libya katika mji wa Derna wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo amesema kuwa, operesheni ya kuukomboa mji huo kutoka mikononi mwa genge moja la kigaidi ilianza rasmi jana (Jumatatu).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 08, 2018 01:26 UTC
  • Operesheni ya kuukomboa mji wa Derna yaanza nchini Libya

Kamanda wa timu ya operesheni ya jeshi la Libya katika mji wa Derna wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo amesema kuwa, operesheni ya kuukomboa mji huo kutoka mikononi mwa genge moja la kigaidi ilianza rasmi jana (Jumatatu).

Salem al-Rifadi, kamanda wa brigedi ya Omar al Mukhtar katika mji wa Derna amesema kuwa, jeshi la Libya jana lilianzisha rasmi operesheni ya kuukomboa mji huo kwa amri wa Jenerali Khalifa Haftar, mkuu wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya.

Abdul Karim Sabra, mtatibu wa brigedi hiyo ya Omar al Mukhtar amewataka wakazi wa mji huo kushirikiana na jeshi hilo hadi magaidi wote watakapofurushwa.

Libya haijawahi kushuhudia utulivu hata siku moja tangu mwaka 2011 wakati Marekani na nchi za Magharibi zilipoivamia kijeshi nchi hiyo

 

Kwa muda mrefu sasa mji wa Derna wa kaskazini mashariki mwa Libya unadhibitiwa na kundi la kigaidi linalojiita kwa jina la Baraza la Mujahid wa Derna, ambalo ni moja ya matawi ya mtandao ya kigaidi wa al Qaida huko nchini Libya.

Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kuung'oa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Marekani na nchi za Magharibi ziliivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, zikafanya uharibifu wa kupindukia kwenye miundombinu ya nchi hiyo na baadaye kuitelekeza nchi huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi hasimu. Tangu wakati huo hadi leo hii Libya haijawahi kushuhudia utilivu hata siku moja kutokana na kila kundi kuendelea kupigania nafasi kubwa zaidi nchini humo.