Kamanda mwandamizi wa FDLR akamatwa na polisi ya Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4441-kamanda_mwandamizi_wa_fdlr_akamatwa_na_polisi_ya_uganda
Kamanda mwandamizi wa kundi la waasi wa Rwanda la FDLR amekamatwa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 05, 2016 02:44 UTC
  • Kamanda mwandamizi wa FDLR akamatwa na polisi ya Uganda

Kamanda mwandamizi wa kundi la waasi wa Rwanda la FDLR amekamatwa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Fred Enanga, msemaji wa polisi ya Uganda amesema kamanda huyo wa FDLR anayejulikana kama Meja Barack Anan alikamatwa jana na polisi ya nchi hiyo alipokuwa akijaribu kuiomba serikali ya Kampala impe hifadhi; na kwa sasa anazuilia katika kituo cha polisi cha Old Kampala. Enanga amesema kamanda huyo wa FDLR anatuhumiwa kuwashawishi wakimbizi walioko katika kambi ya Nyakivale wajiunge na kundi hilo la waasi. Imearifiwa kuwa aghalabu ya wakimbizi hao ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Polisi ya Uganda kwa sasa inashirikiana na Polisi ya Kimataifa Interpol, ili kujua iwapo kamanda huyo mwandamizi wa FDLR atarejeshwa Rwanda au la, licha ya vyeti vya usafiri kuwa vya Kongo DR. Meja Barack Anan anadaiwa kuwa mfuasi kindakindaki wa kundi la waasi wa FDLR tangu mwaka 2000.

Viongozi kadhaa wa kundi la waasi wa Kihutu wa FDLR wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994, ambapo kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa Watusi na baadhi ya Wahutu wenye misimamo ya wastani wasiopungua laki nane waliuawa katika mauaji hayo yaliyojiri kwenye kipindi cha siku mia moja nchini humo.