Mamia ya wahajiri haramu waokolewa katika pwani za magharibi mwa Libya
Wahajiri haramu wapatao 340 raia wa nchi tofauti za Afrika wameokolewa katika pwani za magharibi mwa Libya.
Katika operesheni tatu tofauti zilizofanywa na gadi ya pwani ya Libya wahamiaji haramu 334 waliokolewa hapo jana katika pwani za magharibi mwa nchi hiyo.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa 2018, jumla ya wahajiri haramu elfu nne wameokolewa katika pwani za Libya.
Hapo kabla, Muhammad Bashar, mkuu wa idara ya kupambana na uhajiri haramu nchini Libya alitangaza kuwa kuna wahajiri haramu zaidi ya elfu nane ambao wamepatiwa hifadhi katika maeneo 26 nchini humo.
Libya ndicho kivuko na njia muhimu zaidi inayotumiwa na wahajiri wa nchi za Kiafrika katika safari yao ya kuelekea Ulaya.
Kwa kuitumia hali mbaya ya machafuko na kukosekana amani na uthabiti nchini Libya, wafanyamagendo ya binadamu kila mwaka husafirisha makumi ya maelfu ya wahajiri haramu ili kuwapeleka Ulaya kwa kupitia Libya mkabala wa kupatiwa kitita kikubwa cha fedha. Idadi kubwa ya wahajiri hao hufia njiani kabla ya kufika wanakoelekea.../