Qatar kuendelea kuisaidia Somalia huku mgogoro na Imarati ukitokota
(last modified Tue, 15 May 2018 13:44:21 GMT )
May 15, 2018 13:44 UTC
  • Qatar kuendelea kuisaidia Somalia huku mgogoro na Imarati ukitokota

Qatar imeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Somalia za kurejesha uthabiti na uhuru wa kujitawala huku mgogoro kati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na Umoja wa Falme za Kiarabu ukiendelea kutokota.

Hayo yamesemwa na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani katika mazungumzo yake na Rais Mohammad Abdullahi Farmajo wa Somalia aliyeko ziarani katika nchi hiyo ya Kiarabu na kuongeza kuwa, uhusiano kati ya Doha na Mogadishu umejengeka katika misingi ya udugu na heshima.

Sheikh Tamim amesema, "Qatar itaendelea kuunga mkono jitahada za kurejesha amani, uthabiti na uhuru wa kujitawala Somalia, sambamba na kuimarisha maisha ya Wasomalia."

Mapema mwezi huu, serikali ya Doha iliipa Somalia msaada wa dola milioni 385 za Marekani zitakazotumika katika kuimarisha miundomsingi, elimu na misaada ya kibinadamu.

Rais Mohammad Abdullahi Farmajo wa Somalia

Hii ni katika hali ambayo, Mogadishu ilitangaza hivi karibuni kufuta makubaliano ya kijeshi kati yake na Abu Dhabi, mbali na kuzuia mamilioni ya dola zilizodaiwa kuingizwa nchini Somalia na ndege ya Imarati kinyume cha sheria.

Serikali ya Somalia imekataa kujiunga na Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri katika kuitenga Qatar kwenye mgogoro unaotokota wa Ghuba ya Uajemi, hatua ambayo inaonekana kuzikasirisha tawala hizo ambazo sasa zinalenga kuidhoofisha serikali hiyo.

Hivi karibuni Somalia ililalamikia vikali hatua ya Imarati ya kutia saini mkataba wa kijeshi na kibiashara na eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland.

Tags