Sheikh Zakzaky apandishiwa kizimbani jimboni Kaduna
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna.
Katika kikao cha jana Jumanne, Jaji Kiongozi wa mahama hiyo alimtaka Zakzaky na mkewe kuwasilisha maombi rasmi ya maandishi ya kutaka kuachiwa huru kwa dhamana.
Kesi hiyo imeakhirishwa hadi Juni 21, na wawili hao wamerejeshwa mjini Abuja.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Zeenah Ibrahim, mke wa Sheikh Zakzaky, aliye pia korokoroni, alisema mwanazuoni huyo maarufu amesisitiza kuwa hatasitisha harakati zake za miongo mingi katika Harakati ya Kiislamu, kama sharti la kuachiliwa huru aliyopewa na serikali.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walijeruhiwa vibaya na kukamatwa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria tarehe 13 Disemba 2015 katika Husainia ya mji wa Zaria huko Kaduna, kaskazini mwa Nigeria. Mamia ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky waliuliwa shahidi katika uvamizi huo wa jeshi la Nigeria.
Ijapokuwa muda mfupi baadaye, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe, lakini hadi hivi sasa jeshi na serikali ya nchi hiyo inaendelea kukaidi amri hiyo ya mahakama.