Watu 9 wauawa katika mapigano mapya mashariki mwa Libya
Watu 9 wameuawa kwenye mapigano baina ya jeshi la Libya na magenge ya kigaidi katika mji wa Derna wa mashariki mwa nchi hiyo.
Duru za hospitali zimetangaza leo kuwa, zaidi ya watu 10 wamejeruhiwa katika mapigano hayo mbali na kuuawa watu hao 9.
Kabla ya hapo jeshi la Libya lilikuwa limetangaza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwatia mbaroni magaidi 21 baada ya kuzuka mapigano makali katika mji huo wa Derna.
Tarehe 7 mwezi huu wa Mei, jeshi la Libya lilianzisha operesheni ya kuukomboa mji wa Derna kwa amri ya Jenerali Khalifa Haftar. Operesheni hiyo ilianza kwa mashambulizi makali dhidi ya maficho ya magenge ya kigaidi mjini humo.
Mji wa Derna umo mikononi mwa genge moja la kigaidi linaloitwa Baraza la Mujahidi wa Derna, tawi la mtandao wa al Qaida, tangu mwezi Februari 2011 sambamba na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kuivamia kijeshi Libya katika kampeni za kuupindua utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.
Tangu mwaka huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kushuhudia utulivu na amani hata siku moja kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na nchi za Magharibi dhidi ya miundombinu yake na baadaye kuitelekeza nchi hiyo huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi mengi hasimu ambayo kila moja lina uchu wa kuwa na nguvu zaidi nchini humo.