Hatua za kiusalama zachukuliwa kukabiliana na genge la Daesh nchini Libya
Viongozi wa serikali ya Libya wametangaza kuchukua hatua zaidi za kiusalama kwa ajili ya kukabiliana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ndani ya nchi hiyo.
Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimewanukuu viongozi wa serikali ya Libya wakisema kuwa, hatua za kiusalama kwa ajili ya kukabiliana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ikiwemo miji ya Sirte na Bengazi, kaskazini mwa nchi, tayari zimechukuliwa.
Licha ya kwamba kundi hilo mwishoni mwa mwaka 2016 lilipoteza ngome zake nyingi nchini humo sambamba na kutangazwa kuhitimishwa shughuli za genge hilo nchini Libya, lakini hadi sasa limeendelea kutekeleza hatua zake za kigaidi. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ambalo linaundwa na wanachama kutoka nchi tofauti ikiwemo Libya, hivi karibuni lilifanya jinai mpya za umwagaji damu kwa kutekeleza miripuko kadhaa ya kutegwa ndani ya gari mashariki mwa mji wa Sirte ambayo ni ngome ya vikosi vya kamandi kuu ya jeshi la Libya, na kusababisha mauaji ya watu kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa viongozi wa usalama wa Libya, askari wa serikali mjini Sirte wamejiandaa kukabiliana na mabaki ya wanachama wa kundi hilo lenye misimamo ya Uwahabi. Magaidi wa Daesh waliivamia Libya baada ya kushindwa na kufurushwa nchini Iraq na Syria, suala lililowafanya kukimbilia kaskazini mwa Afrika.