Sudan yalalamikia udhalilishaji wa Misri
Uhusiano baina ya Misri na Sudan umezidi kuharibika baada ya Khartoum kuilalamikia Cairo kuwa inafanya udhalilishaji dhidi yaWamisri waishio nchini Sudan.
Hasira za serikali ya Khartoum ni kubwa kiasi kwamba, wizara ya mambo ya nje ya Sudan imemwita balozi wa Misri mjini humo kumkabidhi malalamiko yake makali baada ya Cairo kurusha hewani mfululizo wa mchezo wa televisheni unaozungumzia waasi wa Misri waishio nchini Sudan.
Mfululizo huo wa mchezo wa televisheni unaojulikana kwa jina la Abu Amr al Masry unarushwa hewani na televisheni ya ON TV ya satalaiti kutokea nchini Misri. Wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema, mchezo huo wa televisheni unawadhalilisha Wamisri waishio nchini humo na vile vile unavuruga imani na uhusiano baina ya watu wa nchi hizo mbili.
Vile vile wizara hiyo ya mambo ya nje ya Sudan imeitaka Misri iache kufanya mambo yatakayozidi kuharibu uhusiano wa pande mbili.
Inaonekana kwamba Sudan imekasirishwa na fikra iliyoenea kwamba makundi yenye silaha ya Misri yanaendesha harakati zao kutokea Sudan. Fikra hiyo imeenea baada ya kuripotiwa kwamba kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Osama bin Laden na wanachama wa makundi mengine yenye silaha walikuwa na maficho yao nchini Sudan katikati ya miaka ya 1990.
Uhusiano baina ya Misri na Sudan si mzuri tangu mwaka jana baada ya rais wa Sudan Omar al Bashir kuyatuhumu mashirika ya kijasusi ya Misri kuwa yanawaunga mkono waasi wanafanya machafuko katika jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan.