Magaidi 8, askari 2 wa Misri wauawa katika mapigano eneo la Sinai
Jeshi la Misri limetangaza habari ya kuuawa askari wake wawili katika mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika eneo la Sinai.
Shirika la habari la AFP limenukuu taarifa ya Jeshi la Misri ikisema kuwa, makabiliano hayo yalitokea jana Jumanne kaskazini mwa Rasi ya Sinai, ambapo pia askari wanne walijeruhiwa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanachama wanane wa Daesh wameangamizwa katika makabiliano ya risasi na jeshi la Misri hapo jana.
Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya Jeshi la Misri kutangaza habari ya kuangamizwa magaidi 19 katika operesheni iliyofanywa na jeshi la nchi hiyo katika Peninsula ya Sinai.
Mwezi Februari mwaka huu, jeshi la Misri kwa kushirikiana na polisi lilianzisha operesheni ya pamoja inayojulikana kwa jina la 'Sinai 2018' kwa shabaha ya kuyasafisha magenge ya kigaidi katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi.
Duru za habari zimeeleza kuwa, magaidi wasiopungua 280 wameshauwa tangu ilipoanza operesheni hiyo, na watu 4467 wameshatiwa mbaroni. Kadhalika jeshi la Misri limepoteza askari wake karibu 40 katika operesheni hiyo.