UN yawawekea vikwazo vigogo 6 kwa kuhusika na magendo ya binadamu Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45566-un_yawawekea_vikwazo_vigogo_6_kwa_kuhusika_na_magendo_ya_binadamu_libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwawekea vikwazo vigogo sita wanaotuhumiwa kuhusika na biashara haramu ya magendo ya binadamu nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2018 02:23 UTC
  • UN yawawekea vikwazo vigogo 6 kwa kuhusika na magendo ya binadamu Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwawekea vikwazo vigogo sita wanaotuhumiwa kuhusika na biashara haramu ya magendo ya binadamu nchini Libya.

UNSC imesema, watu hao ambao ni Mus’Ab Abu-Qarin, Mohammed Kachlaf, Abd Al Rahman Al-Milad, Ermias Ghermay, Fitiwi Abdelrazak na Ahmad Oumar Al-Dabbashi watazuiwa kusafari popote duniani, mbali na mali zao kuzuiliwa, kwa kuhusika na biashara ya kuuzwa wahajiri wa Kiafrika kama bidhaa sokoni.

Haya yanajiri chini ya wiki tatu baada ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UHNCR kutangaza kuwa, wahajiri 12 wameuawa kwa kupigwa risasi na wafanya magendo ya binadamu, walipokuwa wakijarabu kukimbia kambini nchini Libya. 

Wahajiri wa Kiafrika wakiuzwa kama bidhaa Libya

Tukio hilo la Mei 23 lilijiri baada ya kundi la wahajiri 200 kujajaribu kutoroka katika kambi moja walikokuwa wameshikwa mateka katika mji wa Bani Walid, ulioko yapata kilomita 170 kusini mashariki mwa Tripoli.

Libya ni kituo kikuu cha wahamiaji haramu hasa wa Kiafrika wanaokimbilia barani Ulaya. Magenge ya kigaidi na ya magendo ya binadamu yanatumia ukosefu wa amani na kutokuweko serikali kuu yenye nguvu nchini Libya kufanya uhalifu huo.