Mpinzani wa Sassou Nguesso akubali kushindwa katika uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4618-mpinzani_wa_sassou_nguesso_akubali_kushindwa_katika_uchaguzi_wa_rais
Guy-Brice Parfait Kolelas, mgombea wa chama cha upinzani katika Jamhuri ya Kongo ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Rais, hatimaye amekiri kushindwa kwenye uchaguzi huo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 08, 2016 02:33 UTC
  • Mpinzani wa Sassou Nguesso akubali kushindwa katika uchaguzi wa rais

Guy-Brice Parfait Kolelas, mgombea wa chama cha upinzani katika Jamhuri ya Kongo ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa Rais, hatimaye amekiri kushindwa kwenye uchaguzi huo.

Kolelas amewataka wafuasi wake wakubali matokeo ya uchaguzi wa Machi 20 nchini Kongo Brazaville licha ya kuripotiwa kufanyika udanganyifu. Mahakama ya Katiba ya Kongo tarehe 4 mwezi huu ilimtangaza Denis Sassou Nguesso kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais baada ya kupata karibu asilimia 60 ya kura zote za wananchi.

Uchaguzi wa Rais uliofanyika hivi karibuni nchini Kongo Brazaville, ulikuwa wa kwanza kuwahi kufanyika nchini humo kwa mujibu wa katiba mpya ya nchi hiyo. Tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka jana karibu asilimia 90 ya wananchi wa Jamhuri ya Kongo waliipigia kura ya ndio rasimu ya katiba mpya ya nchi yao kupitia kura ya maoni. Katiba hiyo mpya imemuandalia Denis Sassou Nguesso uwanja wa kugombea kiti cha rais kwa mara ya tatu licha ya kura hiyo ya maoni kutajwa na wapinzani wake wa kisiasa kuwa ni sawa na mapinduzi.

Kama ilivyokuwa imetabiriwa, mwezi Januari mwaka huu chama tawala nchini Kongo cha Labor kilimtangaza Denis Sassou Nguesso kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa Rais wa mwezi Machi. Wanaharakati wa kisiasa na vyama vya upinzani vya Kongo pia viliwaarifisha wagombea wao katika uchaguzi huo. Mbali na Denis Sassou Nguesso kuungwa mkono na chama tawala, alikuwa pia akiungwa mkono na vyama vingine saba vya kisiasa. Hatua ya vyama hivyo saba ya kutangaza uungaji mkono wao kwa Nguesso ilimaanisha ushindi wa mapema wa kiongozi huyo.

Ghasia za kisiasa ziliikumba Kongo Brazaville wiki moja baada ya kutangazwa matokeo ya awali ambapo Nguesso alikuwa akiongoza mbele ya wapinzani wake wanane. Wagombea watano wa mrengo wa upinzani uliokuwa ukiipinga serikali walisisitiza kuwa, uchaguzi huo wa Rais uligubikwa na wizi wa kura na kwamba wanataraji kuwasilisha malalamiko yao katika Mahakama ya Katiba.

Wakati huo huo mji wa bandari wa Point Noire ambao ni makao makuu ya kiuchumi ya Jamhuri ya Kongo na kituo cha uzalishaji wa mafuta nchini, ulikumbwa na ghasia na machafuko baada ya kutiwa mbaroni wapinzani wa kisiasa. Askari usalama wa Kongo waliwatia nguvuni baadhi ya wapinzani mjini Brazaville na wengine katika mji wa Point Noire, ambao ni kao makuu ya shughuli za mirengo ya wapinzani wa serikali.

Andre Okombi Salissa na Jean Marie Michel Mokoko pia ambao walikuwa wagombea binafsi wa kiti cha rais huko Kongo, ni miongoni wa watu waliotiwa nguvuni na askari usalama.

Hatua ya mpinzani wa Nguesso ya kukubali matokeo ya uchaguzi wa Rais wa mwezi Machi mwaka huu huko Kongo, ambaye ashika nafasi ya pili katika uchaguzi huo, ni hatua moja mbele katika njia ya kuhitimisha hali ya wasiwasi iliyojitokeza nchini Kongo Brazaville.

Pamoja na hayo yote, wanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo ambao walikuwa na matumaini makubwa ya kubadilishwa uongozi baada ya chama tawala cha Labour kusalia madarakani kwa miaka 32 chini ya uongozi wa Denis Sassou Nguesso, huwenda wakatumia madai ya kufanyika udanganyifu wakati wa uchaguzi ili kuendeleza maandamano dhidi ya serikali.