Makahama ya Misri yaakhirisha hukumu ya watuhumiwa wa Medani ya Rabia
Mahakama ya Jinai ya Cairo leo Jumamosi imeamua kuakhirisha hukumu ya mwisho dhidi ya watu 739 walioshiriki katika maandamano ya mwaka 2013 ambayo yalisambaratishwa kwa mabavu na vyombo vya usalama na kusababisha moja kati ya mauaji makubwa zaidi ya raia katika historia ya sasa ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo imesema uamuzi huo umechukuliwa kwa sababu za kiusalama na kwamba watuhumiwa hawawezi kufikishwa mahakamani.
Kesi hiyo ambayo inawashirikisha pia viongozi wa harakati iliyopigwa marufuku ya Ikhwanul Muslimin akiwemo kinara wake, Mohamed Badie inahusiana na maandamano ya mwaka 2013 yaliyofanywa na wafuasi wa Ikhwanul Muslimin kumuunga mkono Mohamed Morsi aliyekuwa ameondolewa madarakani na jeshi la Misri.
Baadhi ya watuhumiwa huwenda wakakabiliwa na adhabu ya kifo. Kesi hiyo inapingwa vikali na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, fikra ya kuwahukumu watu zaidi ya 700 katika siku moja na wote wakikabiliwa na adhabu ya kifo ni ya kidhalimu na inakiuka hata katiba ya Misri yenyewe.
Zaidi ya raia elfu moja waliuawa kwa kupigwa risasi wakati askari usalama wa serikali ya Cairo walipovamia maandamano ya amani katika Medani ya Rabia al Adawiyya na mengine katika eneo la Giza.