Machafuko ya karibunii Libya yaathiri vibaya uchumi wa nchi
(last modified Tue, 03 Jul 2018 03:07:57 GMT )
Jul 03, 2018 03:07 UTC
  • Machafuko ya karibunii Libya yaathiri vibaya uchumi wa nchi

Shirika la Taifa la Mafuta la Libya limetangaza kuwa mapigano ya hivi karibuni katika eneo la Hilali ya Mafuta nchini humo yamesababisha hasara ya mamilioni ya dola kwa uchumi wa nchi hiyo.

Mustafa Sonallah Mkuu wa Shirika la Taifa la Mafuta la Libya amesema kuwa hadi kufikia sasa kumepatikana hasara ya dola milioni 650 tangu kushambuliwa eneo la Hilali ya Mafuta nchini humo tarehe 14 mwezi Juni mwaka huu.  

Shirika hilo limeongeza kuwa hakuna uwezekano wa kupakia mafuta kutoka katika bandari mbili za al Sadra na Ras Lanuf kwa sababu vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar kamanda wa kikosi kwa jina la Jeshi la Taifa la Libya vinazuia meli kupakia mafuta. Mkuu wa Shirika la Taifa la Mafuta la LIbya ameongeza kuwa hifadhi za mafuta zimejaa na kwamba kwa sasa hakuna uwezekano wa kuzalishwa mafuta mengine kutokana na kutoruhusiwa kupakia mafuta yanayozalishwa. 

Mapigano kati ya makundi yenye silaha na wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar kwa jina la Jeshi la Taifa la Libya yalishuhudiwa wiki kadhaa zilizopita katika eneo la Hilali ya Mafuta nchini humo; ambapo baadhi ya visima vya kuhifadhia mafuta vilichomwa moto.  

Kisima cha mafuta cha Ras Lanuf kilichochomwa moto katika mapigano huko Libya