ICC yatoa waranti nyingine ya kukamatwa kamanda wa jeshi la Libya
Kwa mara nyingine tena, majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wametoa waranti ya kutiwa nguvuni kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya (LNA) anayetuhumiwa kuua makumi ya wafungwa wa kitakfiri.
Majaji hao wamesema wana sababu za msingi za kuamini kwamba, Mahmoud Mustafa Busayf al-Werfalli yeye binafsi aliwaua kwa kuwapia risasi watu 10, mbele ya Msikiti wa Bi’at al-Radhwan mjini Benghazi mnamo Januari 24 mwaka jana; hilo likiwa ni tukio la nane lenye uzito wa jinai za kivita kuhusishwa na kamanda huyo.
Agosti mwaka jana, waendesha mashtaka wa ICC walitoa waranti ya kwanza ya kukamatwa Mahmoud al-Werfalli, wakisisitiza kuwa aliua na kuamuru mauaji ya wafungwa katika matukio saba yakiwemo ya kuua wafungwa 33 miezi ya Juni na Julai mwaka huo katika jela iliyoko karibu na mji wa Benghazi.
Umoja wa Mataifa pia ulilitaka Jeshi la Taifa la Libya kumsimamisha kazi Mahmoud al-Werfalli baada ya kusambazwa mkanda wa video uliomuonesha kamanda huyo wa jeshi la Libya akiwapiga risasi na kuwaua watu watatu waliokuwa wamepiga magoti na kuangalia ukutani wakiwa wamefungwa mikono nyuma ya migongo yao.
Mwezi Juni mwaka jana pia, kulioneshwa mikanda mingine miwili ya video ya mauaji yaliyofanywa na wapiganaji wa jeshi la LNA kwa amri ya al-Werfalli.
Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linalodhibiti maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo limekuwa likifanya jitihada za kueneza satua na ushawishi wake katika maeneo ya katikati na kusini mwa nchi hiyo.