Ikhwanul Muslimin wakanusha kufanya mazungumzo ya siri na serikali ya Misri
(last modified Sat, 07 Jul 2018 04:39:08 GMT )
Jul 07, 2018 04:39 UTC
  • Ikhwanul Muslimin wakanusha kufanya mazungumzo ya siri na serikali ya Misri

Msemaji wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri amekanusha habari ya kufanyika mazungumzo ya siri baina ya harakati hiyo kubwa zaidi ya kisiasa ya upinzani na serikali ya nchi hiyo.

Tal'at Fahmi amekanusha habari ya kuwepo mazungumzo ya siri baina ya pande hizo mbili kwa ajili ya kufikia mapatano na kusema kuwa, habari hizo zilizotangazwa na vyombo vya habari vya Kiarabu na vya kimataifa hazina ukweli wowote.

Fahmi ambaye yeye mwenyewe amewekwa kwenye orodha ya magaidi ya serikali ya Abdul Fattah al Sisi ameongeza kuwa, hakuna uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya siri baina ya Ikwanul Muslimin na serikali ya sasa ya Cairo. 

Harakati ya Ikhwanul Muslimin ambayo ndio kundi kubwa zaidi la kisiasa la upinzani nchini humo ilipigwa marufuku na kuwekwa katika orodha ya makundi ya kigaidi baada ya kuondolewa madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi mwaka 2013.

Muhammad Mursi anashikiliwa katika jela ya Misri

Misri imekuwa uwanja wa ghasia na machafuko ya mara kwa mara tangu mwaka 2013 wakati jeshi la nchi hiyo likiongozwa na Rais wa sasa Abdul Fattah al Sisi, lilipomuondoa maradakani rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia, Muhammad Mursi. 

Tags