Indhari kuhusu mgogoro wa chakula katika eneo la Sahel Afrika
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetahadharisha kuhusu mgogoro wa chakula katika eneo la Sahel barani Afrika.
Shirika la WFP lenye mfungamano na Umoja wa Mataifa limeashiria hali mbaya ya usalama katika eneo la Sahel barani Afrika na kutahadharisha kuwa, mahitaji ya chakula kwa wakazi wa eneo hilo yanaongezeka siku baada ya siku kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo kwa kadiri kwamba, hivi sasa watu milioni sita katika eneo hilo wanakabiliwa na mgogoro wa chakula na wanahitaji misaada ya haraka ili kuweza kuishi.
William Affif Mratibu wa kieneo wa misaada ya dharura wa shirika la WFP nchini Ivory Coast ametangaza kuwa mizozo ya silaha, mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa mvua na kuongezeka haraka jamii ni miongoni mwa masuala muhimu yanayowazidishia machungu na masaibu wakazi wa eneo la Sahel barani Afrika katika miaka ya karibuni.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa hususan Shirika la Chakula na Kilimo la Duniani (FAO), Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) na baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali zinafanya juhudi za kuwadhaminia mahitaji ya chakula ya haraka raia wa eneo la Sahel na wakati huo huku kuchukua hatua za lazima ili kukabiliana na hali mbaya katika eneo hilo.