Rais Kabila wa Kongo akataa kuonana na balozi wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46679-rais_kabila_wa_kongo_akataa_kuonana_na_balozi_wa_marekani
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema hatakutana wala kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, ambaye anatazamiwa kuitembelea nchi hiyo ya Kiafrika wiki hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2018 02:46 UTC
  • Rais Kabila wa Kongo akataa kuonana na balozi wa Marekani

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema hatakutana wala kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, ambaye anatazamiwa kuitembelea nchi hiyo ya Kiafrika wiki hii.

Lambert Mende, msemaji wa serikali ya DRC amesema, "Kuhusu Nikki Haley, nashangaa kwa nini hatua ya Rais Kabila kukataa kuonana naye linaonekana kama suala la utata. Balozi huyo wa Marekani alikuwa hapa Kinshasa mwezi Oktoba mwaka jana na wakafanya mazungumzo na Rais Kabila kwa takriban dakika 90."

Haijabainika iwapo mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa atalazimika kufuta safari yake hiyo ya kuitembelea Kongo DR au la.

Kadhalika serikali ya Rais Kabila imeakhirisha safari iliyotazamiwa kufanyika wiki hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Musa Faki Mahamat mjini Kinshasa, ikisema kuwa kwa sasa ipo mbioni kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

Rais Joseph Kabila ambaye anaiongoza DRC tangu mwaka 2001

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, Bruno Tshibala, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo hatagombea muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu, kutokana na kile kilichotajwa kama moyo wa kuheshimu katiba ya nchi. 

Kabila alikataa kuachia madaraka baada ya kumalizika muhula wake wa utawala kikatiba mwaka 2016, na mpaka sasa binafsi hajajitokeza hadharani kusema iwapo atagombea au ataachia ngazi baada ya uchaguzi huo wa Disemba.