Uganda yaongeza majeshi katika mpaka na DRC Ziwa Edward
Jeshi la Uganda limetangaza kuongeza idadi ya askari wake wanaolinda doria katika mpaka wa pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Ziwa Edward baada ya kujiri machafuko.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) katika wilaya ya Mbarara, Kapteni Stephen Tumwesigye ameliambia shirika la habari la Xinhua kuwa kikosi cha majini cha UPDF sasa kimeimarisha doria Ziwa Edward ili kudumisha usalama. Amekanusha kuwa kuna hali ya wasiwasi katika ziwa hilo huku akisema kuwa biashara inaendelea kama kawaida.
Mnamo Julai 5 askari mmoja wa Uganda aliuawa na mwingine kujeruhiwa vibaya baada ya watu wasiojulikana kuwavurumishia gurunedi askari waliokuwa katika dora ya kawaida karibu na kijiji cha wavuvi cha Rwenshama katika Ziwa Edward.
Tukio hilo lilijiri miezi miwili baada ya wavuvi sita wa Uganda kutekwa nyara na wanamgambo wa Mai Mai kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika ziwa hilo lililo katika mpaka wa nchi hizo mbili.
Baada ya hapo wanajeshi wa Uganda waliwakamata wavuvi 26 wa DRC ambao wanaaminika kuwa wafuasi wa wanamgambo hao wa Mai Mai.

Wiki iliyopita, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilisema wavuvi wasiopungua 12 raia wa nchi hiyo waliuawa katika mapigano makali yanaoendelea kushuhudiwa kwa siku kadhaa sasa kati ya askari wa majini vya nchi hiyo na Uganda, katika maji ya Ziwa Edward. Mapigano hujiri mara kwa mara katika ziwa hilo kutokana na utajiri wake wa mafuta ya petroli na samaki ambao ni muhimu kwa uchumi wa raia wa nchi hizo mbili.