Wahajiri 8 wakiwemo watoto 6 waaga dunia kwenye kontena Libya
Wahajiri wanane wakiwemo watoto sita wamepoteza maisha baada ya kuishiwa na hewa wakiwa ndani ya kasha la kusafirishia mizigo katika mji wa Zuwara ulioko katika pwani ya magharibi mwa Libya.
Duru za kiusalama katika mji huo zimearifu kuwa, wanane hao walioaga dunia ni miongoni mwa wahajiri 100 waliokuwa wamejazana na kufungiwa kwenye kasha hilo la kusafirisha mizigo kwa njia ya baharini, kwa siku kadhaa.
Habari zaidi zinasema kuwa, wahajiri wengine walionusurika kwenye tukio hilo wamepelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu katika mji huo.
Inaarifiwa kuwa, aghalabu ya wahajiri hao ni raia wa Afrika, lakini pia kuna raia wa nchi za Kiarabu na Pakistan.
Mapema mwezi huu, wahajiri 63 walipoteza maisha baada ya boti yao kuzama katika pwani ya Libya, wakiwa katika jitihada za kuvuka bahari ya Mediterranean na kuingia barani Ulaya kutafuta maisha.
Libya ndio lango kuu linalotumiwa na wakimbizi wanaojaribu kuelekea Ulaya kwa njia ya bahari. Kwa miaka kadhaa sasa wakimbizi wengi wamekuwa wakivuka bahari ya Mediterrania wakielekea Ulaya, ingawaje maelfu miongoni mwao wamepoteza maisha kwa kuzama baharini.