Shakhsia wa Kiafrika: Israel isiruhusiwe kujipenyeza Afrika
Shakhsia mbalimbali walioshiriki Kongamano la Kuiunga Mkono Palestina katika mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott wamesisizia udharura wa nchi za Afrika kutouruhusu utawala wa Kizayuni wa Israel kujipenyeza katika bara hilo; na badala yake ziliunge mkono taifa la Palestina.
Jumbe kutoka nchi 17 zilizoshiriki mkutano huo zimesema nchi zote hususan mataifa ya Afrika zinapaswa kusimama kidete dhidi ya njama za Israel katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu, sambamba na kutoruhusu utawala huo kujipenyeza na kupanua satua zake katika nchi za bara hilo.
Mohammad Mahmud Walad Amat, Mkuu wa Taasisi ya Kuwaunga Mkono Wapalestina ambaye alishiriki mkutano huo amesema bara la Afrika linapaswa kuunga mkono kadhia ya Palestina hadi mwisho.
Naye Osameh Hamdan, Mkurugenzi wa Ofisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Harakati ya Kiislamu ya Palestina Hamas ambaye amehudhuria kongamano hilo mbali na kuishukuru serikali ya Mauritania kwa kuwaunga mkono na kuwapa misaada Wapalestina, lakini pia ametoa mwito kwa serikali ya nchi hiyo kukata uhusiano wake na Israel sanjari na kumtimua balozi wa utawala huo haramu mjini, Nouakchott.
Mapema mwezi huu, Riyad al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina aliziomba nchi za bara la Afrika zitazame upya uhusiano wao na utawala haramu wa Israel, akisisitiza kuwa kadhia ya Palestina ndiyo msingi wa kuwepo amani eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla. Aidha alitilia mkazo udharura wa nchi za Afrika kuonyesha mshikamano wao na taifa linalodhulumiwa la Palestina.