Marais Putin na Ramaphosa wajadili ushirikiano wa pande mbili
Rais Vladimir Putin wa Russia na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wamekutana na kufanya mazungumzo pambizoni mwa mkutano wa kumi wa kundi la BRICS mjini Johannesburg Afrika Kusini.
Katika mazungumzo hayo ya pande mbili, Rais wa Russia alidokeza kuhusu uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya nguvu za nyuklia hata hivyo mwenyeji wake Rais wa Afrika Kusini alisema kuwa Pretoria haiwezi kusaini mkataba kama huo kwa sasa.
Rais wa Afrika Kusini aliongeza kuwa uchumi wa nchi yake umesita hivi sasa haukuwi kama wanavyotaka na kwamba si wakati muafaka sasa kwa nchi hiyo kusaini makubaliano hayo ya nyuklia.
Wakati huo huo Marais hao wawili wa Russia na Afrika Kusini walisaini taarifa ya pamoja ya ushirikiano wa kistratejia kati ya nchi mbili hizo. Vile vile walisaini makubaliano katika sekta ya kilimo na kukuza ushirikiano katika vyanzo vya maji.