Rais wa Misri asaini sheria inayowapa kinga majenerali wa jeshi
Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ameidhinisha sheria inayowapa kinga ya kufikishwa mahakamani majenerali wa jeshi wanaohusishwa na machafuko yaliyotokea baada ya mapinduzi ya Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini humo; siku 10 baada ya Bunge la nchi hiyo kupasisha kwa kishindo muswada wa sheria hiyo.
Baada ya kusaini muswada huo na kuwa sheria hiyo jana Alkhamisi, ilichapishwa katika gazeti rasmi la serikali; na sasa majenerali hao watakuwa na kinga maalumu kama ya wanadiplomasia.
Sheria hiyo inampa Rais Abdul Fattah al-Sisi haki ya kuteua majenerali wanaopaswa kupewa tuzo na kinga ya kufikishwa mahakamani kutokana na uhalifu liofanyika kuanzia Julai 3 mwaka 2013 hadi tarehe 8 Juni 2014, kipindi ambacho rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia wa Misri, Mohamed Mursi aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya jeshi.
Mamia ya raia waliuawa wakati askari usalama wa serikali ya Cairo walipovamia Medani ya Rabia mjini Cairo Agosti mwaka 2013.
Makundi mbalimbali ya kisiasa na kijamii nchini humo kama vile harakati ya Ikhwanul Muslimin, yamekosoa vikali sheria hiyo.
Zaidi ya raia elfu moja waliuawa kwa kupigwa risasi wakati askari usalama wa serikali ya Cairo walipovamia maandamano ya amani katika Medani ya Rabia al Adawiyya na maeneo mengine katika eneo la Giza.