Nchi za kati na magharibi mwa Afrika zajadili tishio la ugaidi
Nchi 26 za kanda ya kati na magharibi mwa Afrika zimekutana kujadili ugaidi na tishio la usalama katika eneo hilo.
Mkutano huo umefanyika katika mji mkuu wa Togo, Lome na kuwaleta pamoja viongozi na wawakilishi wa nchi 15 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS)- na Jumuiya ya Kiuchumi ya Kati mwa Afrika (ECCAS).
Taarifa iliyotoelewa baada ya kumalizika mkutano huo Jumanne ya leo imesema nchi ilizoshiriki zimejadili hali ya usalama katika nchi za kati na magharibi mwa Afrika na changamoto zitokanzao na ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya silaha na uhalifu katika mitandao ya intaneti.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais Faure Gnassingbe wa Togo amesema kuna haja ya nchi za eneo hilo kushirikiana zaidi katika kulinda mipaka yao ili kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa Afrika Magharibi Muhammad Ibn Chambers amesema nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana zaidi katika kukabiliana na mizizi na vyanzo vya ukosefu wa usalama na ugaidi.
Aidha ametoa wito wa kufanyika jitihada maradufu kuokoa eneo la Ziwa Chad kutokana na hali mbaya ya ukame katika eneo hilo ambayo imepelekea maisha ya wakulima na wafugaji kuwa magumu sana.