Kuteuliwa msuluhishi kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo ya kitaifa Kongo DR
Umoja wa Afrika (AU) umemteuwa mpatanishi ili kuanisha jitihada za kufanyika mazungumzo ya kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Nkosazana Dlamini Zuma, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amemteuwa Edem Kodjo, waziri mkuu wa zamani wa Togo kuwa msuluhishi katika mazungumzo ya kitaifa ya Kongo.
Bi Dlamini Zuma ameeleza katika taarifa aliyotoa kwamba uteuzi huo umefanyika ili kusaidia mchakato wa mazungumzo ya kitaifa lengo likiwa ni kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayohusiana na uchaguzi mkuu ujao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Zuma ameongeza kuwa, uteuzi huo umefanyika sambamba na ahadi zilizotolewa kupitia taarifa ya pamoja ya Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kifaransa (OIF) mnamo tarehe 16 mwezi Februari mwaka huu, ambayo ilisisitiza kuendelezwa misaada kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika pia amewataka wapinzani na serikali ya Kongo washirikiane na msuluhishi Edem Kodjo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza mwezi Februari mwaka jana kuwa, uchaguzi wa rais na bunge wa nchi hiyo utafanyika Novemba 27 mwaka huu. Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kongo, Corneille Nangaa alisema mwezi Februari mwaka huu kuwa kuna masuala ndani ya katiba ya nchi hiyo yanayozuia kufanyika uchaguzi wa rais katika muda ulioainishwa, na kwa msingi huo ni jambo lisilowezekana kufanyika uchaguzi huo kama ilivyopangwa. Nangaa amesema kuwa matatizo ya kiufundi yanayohusiana na kuhakikiwa daftari la wapiga kura na misaada ya kifedha kwa ajili ya kusaidia mwenendo wa uchaguzi, yote hayo yanaweza kusababisha kuakhirishwa zoezi la uchaguzi kwa miezi isiyopungua 16.
Viongozi wa serikali ya Kongo na Rais Kabila mwenyewe kwa muda sasa wamekuwa wakizungumzia suala la kuwepo matatizo katika mchakato wa zoezi la uchaguzi ujao wakisisitiza kuwa zoezi hilo linahitajia muda zaidi.
Katika upande mwingine wapinzani wa serikali ya Kongo wanaamini kuwa serikali inatoa visingizio hivyo ili kukwamisha kufanyika uchaguzi mkuu katika wakati uliopangwa na kutoa mwanya kwa Rais Joseph Kabila wa kusalia madarakani. Suala hilo limekuwa likizidisha mashinikizo na wimbi la upinzani dhidi ya Rais Kabila; kiasi kwamba kiongozi huyo siku kadhaa zilizopita alitoa wito wa kufanyika mazungumzo kati ya serikali na wapinzani. Hata hivyo vyama vya upinzani vimekataa kuketi kwenye meza ya mazungumzo.
Wakati huo huo muda wa kuhudumu kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za kurejesha amani na kuheshimiwa haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umerefushwa zaidi. Hata hivyo kuna wasiwasi kwamba kuongezeka mashinikizo, mgogoro na machafuko mapya nchini humo, kutazidisha changamoto za kiusalama na kisiasa katik nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kwa kuzingatia migogoro inayozisumbua baadhi ya nchi za Kiafrika na kuongezeka mivutano ya kisiasa katika nchi hizo, Umoja wa Afrika unafanya jitihada za kutekeleza siasa za kistratejia kupitia njia ya kufanyika mazungumzo na juhudi za usuluhishi ili kuzuia vita na mapigano mapya katika nchi hizo.
Kwa msingi huo, kuteuliwa msuluhishi kwa ajili ya mazungumzo ya kitaifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kunapasa kutathminiwa katika uwanja huo.