Askari usalama wavamia jengo la wizara ya mambo ya nje ya Somalia
(last modified Sun, 05 Aug 2018 02:33:32 GMT )
Aug 05, 2018 02:33 UTC
  • Askari usalama wavamia jengo la wizara ya mambo ya nje ya Somalia

Duru za habari Somalia zimeripoti kuwa askari usalama wamevamia jengo la Wizara ya Mambo ya Nje katika mji mkuu Mogadishu kwa lengo la kumtia nguvuni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo.

Gazeti la Al-Somalil-Jadid limeripoti kuwa askari hao wa usalama walivamia jengo hilo jana Jumamosi wakijaribu kumtia nguvuni Mukhtar Mahd Daud ili kumpeleka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo, baada ya askari usalama kuvamia jengo la Wizara ya Mambo ya Nje, yalizuka makabiliano baina yao na walinzi wa naibu waziri huyo lakini hayakutokea maafa yoyote katika patashika hiyo.

Askari wa vikosi vya usalama vya Somalia

Inasemekana kuwa mkuu wa polisi ya Somalia Jenerali Ali Muhammad aliingilia kati kadhia hiyo na baada ya kufanya mazungumzo na naibu waziri wa mambo ya nje na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo mzozo huo ulitatuliwa kwa njia ya amani.

Kabla ya hapo, askari usalama wa Somalia walivamia wakati wa usiku nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Utoaji Misaada  na Idara ya Maafa ya Kimaumbile na kumtia nguvuni afisa huyo kwa tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya wakimbizi wa ndani.../