UN yataka kutatuliwa matatizo ya kiusalama barani Afrika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka taasisi za kimataifa zilizoko barani Afrika kutatua matatizo ya kiusalama katika eneo la Sahel na magharibi mwa bara hilo.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Usalama na UN imeashiria changamoto kubwa za kiusalama huko magharibi mwa Afrika na eneo la Sahel na kutilia mkazo udharura wa kuwepo ushirikiano zaidi baina ya taasisi na jumuiya za kimataifa zilizoko barani humo na serikali za nchi za eneo hilo.
Taarifa hiyo imesema kuwa, ugaidi, uharamia, mapigano ya kikabila na uhalifu wa kupanga unaovuka mataifa ni miongoni mwa changamoto za kiusalama za magharibi na Sahel Afrika.
Katika taarifa hiyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limelaani magendo ya binadamu huko magharibi mwa Afrika na kusema kuwa jinai hiyo imekuwa sababu ya kujitokeza aina nyingine za uhalifu na jinai na kushadidi machafuko katika maeneo hayo.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za magharibi na eneo la Sahel Afrika zimekuwa zikukumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye misimamo mikali na ya kigaidi kama Boko Haram kutokana na changamoto nyingi za kiusalama kama mgogoro wa Mali na mapigano ya ndani katika nchi ya Libya.