Mkuu wa zamani wa polisi nchini Uganda apandishwa kizimbani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47661-mkuu_wa_zamani_wa_polisi_nchini_uganda_apandishwa_kizimbani
Mkuu wa zamani wa polisi nchini Uganda Jenerali Kale Kayihura amefikishwa katika mahakama ya jeshi ya Makindye mjini Kampala baada ya kufunguliwa mashitaka ya kutowajibika katika kazi yake.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Aug 24, 2018 09:36 UTC
  • Mkuu wa zamani wa polisi nchini Uganda apandishwa kizimbani

Mkuu wa zamani wa polisi nchini Uganda Jenerali Kale Kayihura amefikishwa katika mahakama ya jeshi ya Makindye mjini Kampala baada ya kufunguliwa mashitaka ya kutowajibika katika kazi yake.

Jenerali Kayihura anakabiliwa na mashitaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kulinda zana za kivita na kusaidia kurejeshwa nyumbani kinyume cha sheria raia wa Rwanda waliokuweko uhamishoni. Kulingana na nyaraka za mashitaka, kati ya mwaka 2010 na 2018 Kale Kayihura alitoa idhini silaha zitolewe kwa watu wasiostahili

Jenerali Kale Kayihura amekanusha mashitaka dhidi yake akisema kuwa ni madai yasio na msingi. Jenerali Kayihura amekuwa akizuiliwa katika kambi ya kijeshi ya Makindye katika kitongoji cha mji mkuu Kampala, baada ya kukamatwa nyumbani kwake Katebe katika wilaya ya Lyantonde mwezi Juni mwaka huu.

Mawakili wake wameomba aachiliwe huru kwa dhamana, lakini mahakama imewataka wawasilishe ombi hilo kwa maandishi.

Jenerali Kayihura alihudumu kama mkuu wa Polisi kwa takriban miaka 12 kabla ya a kuachishwa kazi na Rais Yoweri Kaguta Museveni.

Kesi yake imeahirishwa hadi tarehe 4 Septemba mwaka huu. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa mkuu huyo wa zamani wa polisi ya Uganda alikuwa akifanya ujasusi kwa maslahi ya nchi jirani ya Rwanda.