Morocco yazuia maelfu ya wahajiri haramu kutumia ardhi ya nchi hiyo
Viongozi wa Morocco wametangaza kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, serikali ya nchi hiyo imefanikiwa kuzuia wahajiri haramu 54 elfu kutumia ardhi ya nchi hiyo kuelekea barani Ulaya.
Viongozi hao wa Morocco pia wamesema, wamefanikiwa kuvunja mitandao 74 ya wahalifu waliokuwa wanaendesha magendo ya wanadamu kama ambavyo pia maafisa usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kukamata boti elfu moja na 900 zilizokuwa zinatumika kusafirisha wahajiri haramu.
Wizara ya mambo ya ndani ya Morocco aidha imesema, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018 hadi hivi sasa, washukiwa 230 wa magendo ya binadamu wameshapandishwa kizimbani nchini humo.
Morocco ambayo ni moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahajiri haramu wanaokimbilia barani Ulaya kutokana na kuwa karibu sana na Uhispania, hivi sasa imeamua kuendesha opereshenei kubwa ya kupambana na magenge ya magendo ya binadamu.
Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Wahajiri limetangaza kuwa, mwaka huu wa 2018 zaidi ya wahajiri 35,000 wameingia nchini Uhispiania kwa njia za magendo.
Mara nyingi wahajiri hao ambao wengi wao ni Waafrika huwa hawafiki wanakokwenda bali huishia mikononi mwa magenge hatari ya magendo ya binadamu na ya kigaidi.