Wanachama 75 wa Ikhwanul Muslimin wahukumiwa kifo nchini Misri
(last modified Sun, 09 Sep 2018 02:21:40 GMT )
Sep 09, 2018 02:21 UTC
  • Wanachama 75 wa Ikhwanul Muslimin wahukumiwa kifo nchini Misri

Mahakama ya rufaa ya Misri imewahukumu adhabu ya kifo wanachama 75 wa kundi la Ikhwanul Muslimin kwa tuhuma za kuhusika katika matukio yanayojulikana kwa jina la "Rābiʿa al-ʿAdawiyya" kama ambavyo pia imewahukumu kifungo cha maisha jela wanachama wengine 46 wa kundi hilo.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, mahakama ya rufaa ya Cairo imetoa hukumu ya kunyongwa wanachama hao 75 wa kundi la Ikhwanul Muslimin baada ya kuidhinishwa na Mufti wa Misri kwa mujibu wa katiba. Watuhumiwa 29 kati ya hao 75 hawakuweko mahakamani.

Wafuasi wa Ikhwanul Muslimin wakiwa jela Misri

 

Mahakama hiyo pia imewafunga maisha jela Mohammed Badie, kiongozi wa kundi la Ikhwanul Muslimin na wanachama wengine 46 wa kundi hilo kwa madai ya kuhusika katika maandamano ya wafuasi wa Mohamed Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia ambaye alipinduliwa na jeshi na baadaye kutiwa mbaroni na kuwekwa kizuizini tangu mwaka 2013 hadi hivi sasa. Wanachama hao wa Ikhwanul Muslimin wanatuhumiwa kuhusika katika maandamano ya kulalamikia kitendo cha jeshi cha kumpindua Mohamed Morsi, maandamano ambayo yalifanyika katika medani mbili za Rābiʿa al-ʿAdawiyya na al Nahdha, mjini Cairo.

Usama Mohamed Morsi, mtoto wa kiume wa Mohamed Morsi amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela huku Muhammad Shawkan, mpiga picha na mwandishi wa habari wa Misri akihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Alama maarufu ya waandamanaji wa Misri iliyong'oa madarakani dikteta wa nchini hiyo Hosni Mobarak

 

Itakumbukwa kuwa, mwaka 2013, wafuasi wa Mohamed Morsi walifanya maandamano makubwa katika medani mbili za Rābiʿa al-ʿAdawiyya na al Nahdha mjini Cairo kulalamikia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na rais wa hivi sasa wa nchi hiyo Abdel Fattah el Sisi. Tarehe 14 Agosti 2013, jeshi la el Sisi aliyekuwa waziri wa ulinzi wa wakati huo liliwavamia waandamanaji katika medani hizo mbili na kuua na kujerumi mamia ya watu.

Tags