Sep 12, 2018 14:10 UTC
  • Sarraj: Uchaguzi hauwezi kufanyika Libya katika mazingira ya sasa

Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amesema ni muhali kufanyika uchaguzi nchini humo katika mazingira ya hivi sasa.

Fayez al Sarraj ameyasema hayo leo Jumatano katika mahojiano na gazeti la Italia la Corriere della Sera na kuongeza kuwa, "Hatuwezi kupiga kura wakati huu ambapo kuna ukosefu wa usalama wa uthabiti mitaani, ni sharti uchaguzi ufanyike katika mazingira ambayo matokeo yake yatakubaliwa na kila mtu."

Ingawaje huko nyuma alitangaza kuunga mkono juhudi za kisiasa za kutatua mgogoro wa nchi yake kupitia uchaguzi wa rais na bunge, lakini kauli yake mpya inatilia shaka uwezekano wa kufanyika uchaguzi huo kabla ya kumalizika mwaka huu.

Sarraj (kushoto), Macron na Khalifa Haftar

Sarraj pamoja na hasimu wake Khalifa Haftar, Kamanda Mkuu wa Jeshi mashariki mwa Libya mwezi Mei mwaka huu walikutana mjini Paris chini ya uenyekiti wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, na wakakubaliana kushirikiana na Umoja wa Mataifa kwa minajili ya kuandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo kufikia Disemba 10 mwaka huu. 

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) mwaka 2011.

Tags