Magaidi 15 waangamizwa Sinai Kaskazini nchini Misri
(last modified Thu, 04 Oct 2018 02:41:41 GMT )
Oct 04, 2018 02:41 UTC
  • Magaidi 15 waangamizwa Sinai Kaskazini nchini Misri

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza habari ya kuangamizwa magaidi 15 katika mapigano baina ya vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo na magaidi hao kaskazini mwa Misri.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema katika taarifa yake ya jana Jumatano kwamba, askari wa nchi hiyo wameshambulia maficho ya magaidi hao katika mji wa al Arish wa mkoa wa Sinai Kaskazini na kuua magaidi 15 katika mapigano yaliyozuka baina yao.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa magaidi hao walikuwa wana nia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi wakati wa sherehe za Oktoba 6 nchini Misri.

Abu Hamza al Maqdisi ambaye magaidi wa Daesh nchini Misri wanadai alikuwa kamanda wao kabla ya kuuawa hivi karibuni

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikosi vya ulinzi vya Misri vimefanikiwa kukamata silaha nyingi katika maficho ya magaidi hao.

Wakati huo huo genge la kigaidi la Daesh (ISIS) juzi Jumanne lilisambaza picha za mtu liliyemtaja kwa jina la Abu Hamza al Maqdisi na kusema kwamba alikuwa kamanda wa genge hilo huko Sinai Misri kabla ya kuuawa hivi karibuni. 

Genge la kigaidi la Ansar Baytul Muqaddas ambalo baada ya kujiunga na magaidi wa Daesh limebadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai limekuwa likifanya mashambulizi mbalimbali ya kigaidi kwa miaka kadhaa sasa nchini Misri.

Tags