Kongo yautuhumu Umoja wa Ulaya kuwa inaingilia uchaguzi nchini humo
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeutuhumu Umoja wa Ulaya kuwa unaingilia uchaguzi ujao wa rais nchini humo kwa kutosikiliza wito wa serikali ya Kinshasa wa kutaka kuondolewa vikwazo kwa mgombea wa kiti cha urais ambaye ni chaguo la Rais Joseph Kabila.
Mgombea huyo kwa jina la Emmanuel Ramazani Shadary alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati Kongo ilipokabiliwa na maandamano dhidi ya hatua ya Rais Kabila ya kukataa kuondoka madarakani baada ya kumalizika muhula wake wa urais mwezi Disemba mwaka 2016. Waandamanaji waliopinga hatua hiyo walikandamizwa vikali na askari usalama. Umoja wa Ulaya umemuwekea vikwazo Ramazani na shakhsia wengine 15 kwa kile ulichokitaja kuwa ukiukaji wa haki za binadamu na kuingilia mchakato wa uchaguzi. Disemba 12 umoja huo unatarajia kupiga kura ili kuongeza muda wa vikwazo hivyo au la.
Uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umepangwa kufanyika Disemba 23. Uamuzi wa Rais Joseph Kabila wa kutogombea katika uchaguzi ujao wa rais umefungua njia kwa kile ambacho kinaweza kuwa mchakato wa kwanza wa mpito wa kidemokrasia kuwahi kushuhudiwa huko Kongo baada ya miongo kadhaa ya utawala usio wa kidemokrasia, mapinduzi na uasi.