Ujumbe wa UN nchini Libya wapongeza utangulizi wa mipango mipya ya kiusalama
Ujumbe wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umepongeza mipango mipya ya kiusalama katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli iliyobuniwa na Baraza la serikali la uongozi.
Umoja wa Mataifa umeeelza kuwa ujumbe wa UNSMIL unakaribisha mchakato huo ulioandaliwa na kamati kuu ya mipango ya usalama ya Tripoli iliyoasisiwa na baraza la serikali la uongozi na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Ujumbe huo wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa huko Libya umebainisha kuwa mpango rasmi kuhusu hali ya usalama uliowasilishwa na Waziri Mkuu Fayez al Sirraj umeweka wazi kuwa makundi yenye silaha yanapaswa kutoka katika taasisi za serikali na mahala hapo kuchukuliwa na vikosi halali vitakavyoidhinishwa na serikali.
Wakati huo huo Ramadan Zarmouh Mkuu wa kamati ya mipango ya usalama wa Libya katika Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi hiyo wiki iliyopita alisema kuwa wanafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mchakato huo wa hatua za kiusalama ili kuhitimisha uwezekano wa kuzuka tena mapigano huko Tripoli.